Nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappé, amemtetea mchezaji mwenzake Vinícius Júnior baada ya mshambuliaji huyo wa Brazil kuzomewa na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya RB Leipzig, uliochezwa jana, Jumatano, Oktoba 21, 2026, kwenye Uwanja wa Santiago Bernabéu.
Alhamisi, Oktoba 22, 2026

Picha na Mtandao
Madrid, Hispania. Nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappé, amemtetea mchezaji mwenzake Vinícius Júnior baada ya mshambuliaji huyo wa Brazil kuzomewa na baadhi ya mashabiki wa timu hiyo wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya RB Leipzig, uliochezwa jana, Jumatano, Oktoba 21, 2026, kwenye Uwanja wa Santiago Bernabéu.
Mbappé alitoa kauli hiyo baada ya Real Madrid kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Leipzig, akisisitiza kuwa licha ya Vinícius kukosolewa na baadhi ya mashabiki, anaamini mshambuliaji huyo alicheza vizuri.
Vinícius alianza mchezo huo akiwa kwenye kikosi cha kwanza pamoja na Mbappé, licha ya kuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi nne katika mashindano ya ndani ya Hispania.
Hata hivyo, katika mchezo huo, nyota huyo wa Brazil alionekana kushindwa kuonyesha makali yake ya kawaida, hali iliyosababisha baadhi ya mashabiki wa Real Madrid kumzomea.
Tukio hilo limeongeza mjadala kuhusu kiwango cha Vinícius na namna anavyopokelewa na mashabiki wa klabu hiyo katika kipindi ambacho anakabiliwa na ukosoaji kutokana na uchezaji wake.
Mbappé, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, aliulizwa kuhusu kitendo cha mashabiki kumzomea Vinícius pamoja na kiwango alichoonyesha dhidi ya Leipzig.
Akijibu, mshambuliaji huyo wa Ufaransa alisema mashabiki hawakumzomea pekee, bali pia walimpigia makofi katika sehemu nyingine za mchezo.
“Bernabéu imemzomea Vini? Lakini pia walimpigia makofi. Kuhusu kiwango chake? Mimi si kocha. Sizungumzii habari za wachezaji wenzangu. Nafikiri alicheza vizuri,” amesema Mbappé.
Kauli hiyo inaonyesha namna Mbappé anavyompa sapoti Vinícius licha ya presha inayomkabili mshambuliaji huyo kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa Real Madrid.
Wachezaji hao wawili ni sehemu muhimu ya safu ya ushambuliaji ya Madrid, huku ushirikiano wao ukitarajiwa kuisaidia timu hiyo katika kampeni za mashindano ya ndani na Ulaya.
Kwa upande wa Vinícius, changamoto iliyopo ni kurejesha kiwango chake cha kawaida na kujibu ukosoaji kwa kuonyesha ubora wake uwanjani. Hata hivyo, kauli ya Mbappé inaonyesha kuwa bado anaungwa mkono na baadhi ya wachezaji wenzake ndani ya kikosi hicho.